Pichani juu nikiwa na Komredi Issa Shivji, Zanzibar, Oktoba, 2006.
WASOMI na wanasiasa mbalimbali wameilaumu Serikali ya CCM kwa kuua Azimio la Arusha na kuanzisha Azimio la Zanzibar lililoua mwelekeo wa taifa. Wakizungumza katika Kongamano la kujadili Azimio la Arusha lililoandaliwa na Chama cha Sauti ya Vijana cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufanyika katika chuo hicho jana, wasomi na wanasiasa hao walionyesha nia ya kutaka azimio hilo lirudishwe na kuwa moja ya misingi ya mabadiliko ya Katiba.
Awali akitoa mada kuhusu Azimio la Arusha, Mwenyekiti wa Kigoda cha Kitaaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema kuwa dalili za kufa kwa Azimio la Arusha zilianza kujionyesha kabla ya Azimio la Zanzibar.
Profesa Shivji alizitaja dalili hizo kuwa ni pamoja na utaifishwaji wa rasilimali za umma, operesheni vijiji iliyotokea mwanzoni mwa miaka ya 1970, vuguvugu la wafanyakazi na hatua ya CCM kushika hatamu. Profesa Shvji ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema pamoja na kufa kwa azimio hilo bado mzimu wake utaendelea kusumbua.
“Walijitokeza watu wenye jazba ndani ya chama na kuhoji uhalali wa Serikali kutaifisha hata maduka, vituo vya kuuzia mafuta. Kwa kawaida Serikali haiwezi kumiliki maduka, lakini walitaka kuichanganya tu ili nao wamiliki,” alisema Profesa Shivji. Akizungumzia kuhusu CCM kushika hatamu kama hatua mojawapo iliyovunja Azimio la Arusha, Profesa Shivji alisema kuwa chama hicho ndiyo kilichoshika mwongozo huku Bunge likiwa mtendaji tu.
“Chama kiliposhika hatamu, kilikuwa chama dola, Bunge lilikuwa na kazi ya kutekeleza tu, viongozi nao walishika ‘utamu’,” alisema.
Kuhusu vyama vya siasa, Profesa Shivji alikumbusha kauli ya Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema kuwa angependa nchi iwe na vyama viwili vikubwa vya upinzani vinavyofuata mfumo wa ujamaa, lakini mpaka sasa karibu vyama vyote vinafuata ubepari.
“Hadi sasa hakuna hata chama kimoja kinachofuata ujamaa na kuwajali wananchi, vyama vyote vinafuata mrengo wa kulia. Hata wakipata matatizo wanakimbilia kwenye balozi za nchi za kibepari,” alisema.
Kuhusu Azimio la Arusha katika mchakato wa Katiba, Profesa Shivji alisema katiba mpya siyo suluhisho, bali maoni ya wananchi pekee ndiyo yanapaswa kuangaliwa zaidi.
Shivji alitanabaisha: “Katiba mpya siyo mwarobaini au kikombe cha Babu wa Loliondo kinachotibu maradhi yote. Kitu cha muhimu ni mchakato, wananchi watatoa malalamiko yao, manung’uniko kulingana na mahitaji yao.”
Akichangia mjadala huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri umuhimu wa Azimio la Arusha na kuhimiza vijana kujitokeza na kulirudisha.
“Leo huwezi kuzungumza historia ya nchi yetu bila kutaja Azimio la Arusha. Kwa kuwa Profesa Shivji amesema kuwa haiwezekanai kulirudisha ila tunaweza kuirejesha misingi yake, basi vijana tujifunge mikanda na kufanya hivyo ili tutoke hapa tulipo,” alisema Nnauye.
Hata hivyo, akihitimisha kongamano hilo, Profesa Shivji alimkosoa Nape akihoji kuwa CCM itawezaje kulirudisha Azimio la Arusha wakati ilishindwa kulitetea?
“Sijui kama bado Nape yupo, lakini alizungumzia kuhusu kulirudisha azimio. Ni kweli sasa CCM wafikirie kulirudisha azimio. Lakini watalirudishaje wakati walishindwa kulisimamia? Ni swali tu najiuliza,” alisema Profesa Shivji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisahihisha dhana iliyojengeka kuwa kulikuwa na Azimio la Zanzibar akisema, “Hakuna Azimio la Zanzibar, ndiyo maana nikasema fanyeni utafiti, siyo mnasimama hapa chuo kikuu na kusema kuwa kulikuwa na Azimio la Zanzibar. Kile kilikuwa ni kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Zanzibar,” alisema Butiku.
Alifafanua kuwa kikao hicho kilipokea maombi ya waliokuwa viongozi wa CCM ambao walilalamika kuwa miiko ya Azimio la Arusha ilikuwa inawafanya kuwa ombaomba, ndipo wakaomba masharti yalegezwe.
Hata hivyo, alisema baada ya kuruhusiwa, ndipo matajiri walipopata mwanya wa kujilimbikizia mali.
Butiku alifahamisha kuwa miiko ya Azimio la Arusha ilikuwa migumu mno kuifuata.
“Miiko ya Azimio la Arusha ilikuwa migumu. Nyie tukiwaletea miiko hiyo mtaimudu?” alihoji Butiku.
Naye Balozi Ibrahim Kaduma, aliyewahi kuwa Waziri wakati wa Mwalimu Nyerere, alisisitiza juu ya umuhimu wa maadili ya uongozi kama njia ya kukomesha ufisadi nchini.
Hata hivyo, Kaduma alimkosoa Profesa Shivji katika suala la maadili aliposema kuwa maadili hayafundishwi darasani bali yanaigwa tu.
“Inawezekana kweli miiko ya Azimio la Arusha haikuwa maadili, lakini lengo lake lilikuwa ni kujenga maadili. Kwa hiyo maadili yanafundishika, yakikomaa yanakuwa utamaduni wa nchi. Mmomonyoko wa maadili ndiyo umeleta rushwa, wizi na ufisadi,” alisema Kaduma.