Sunday, May 1, 2011

Kuuliwa Kwa Osama Bin Laden; Tafsiri Yangu


"Anayeogelea baharini haogopi mvua." Anasema Osama Bin Laden.

Naam, habari zimetufikia, kuwa Kikosi Maalum Cha  WaMarekani kimeendesha opereshani maalum iliyopelekea kuuliwa kwa Osama Bin Laden nchini Pakistani usiku wa kuamkia leo. Ndio, anayeogelea kwenye bahari yenye kina kina kirefu yumo katika hatari ya kuzama ua kuliwa na papa.

Osama Bin Laden ameshauliwa. Tafsiri yangu; huu ni ushindi mkubwa kwa Barack Obama na bila shaka, akiutumia vema, utamwongezea uhakika wa kushinda Urais kwenye Uchaguzi ujao na kuacha historia nyuma yake. Maana, Barack Obama alipoingia madarakani, aliweka bayana, kumtafuta na kumkmaata au kumwua Osama Bin Laden ni ajenda nambari moja katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Obama, chini ya uongozi wake, amefanikisha kile ambacho kilidhaniwa hakiwezekani.

Kuuliwa kwa Osama Bin Laden kunatuambia pia, kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho na kuwa katika dunii hii ya sasa ni vigumu kwa kiongozi wa kisiasa au kikundi cha kigaidi kufanya maovu na kuachwa ajiendee zake. Dunia ikimvalia njuga, basi, itafika siku, atapatikana akiwa hai au amekufa. Kwamba mtenda maovu ana malipo yake hapa hapa duniani.

Na mwaka 2011 utabaki kuwa wa ajabu sana katika historia ya dunia. Ndani ya miezi mitano ya mwaka huu kuna mengi makubwa yametokea; Kuamka kwa Ulimwengu wa Waarabu. Tumeona Tunisia, Misri, Syria, Libya na kwingineko. Na hili la kuuliwa kwa Osama Bin Laden linazidi kutukumbusha umuhimu wa kuangalia ukutani na kusoma alama za nyakati; kuna wengine watapukutika. Ndio, mtaziona ishara.

Na Osama Bin Laden alikuwa na sura mbili tata. Ni zipi hizo? Mtakumbuka, ilikuwa ni mwezi Januari mwaka 2006 wakati Osama Bin Laden alipotoa kauli hiyo akiwa mafichoni. Hiyo ilikuwa ni mara ya mwisho kwa kiongozi huyu wa kikundi cha Al-Qaida kujitokeza tena hadharani na 'kuhutubia" ulimwengu kupitia kituo cha televisheni cha Al-Jaazira. Sauti ya Osama ilikuwa imenaswa kwenye mkanda na kuthibitishwa na wataalam wa sauti katika nchi za Kiarabu na hata CIA, Shirika la ujasusi la Marekani..

Osama alitaka kuulezea msimamo wa Al-Qaida na labda wake mwenyewe wenye kutoa tafsiri nyingi. Kwa kiasi fulani ulimwengu ulishangazwa kwa Osama kuamua kutumia kipindi cha mwanzo wa mwaka ule kuutangazia ulimwengu kuwa bado alikuwa hai na kwamba alikuwa na dhamira ya kuendeleza harakati zake za kigaidi.

Kabla ya Januari 2006, mara ya mwisho kwa ulimwengu kumsikia Osama Bin laden akiongea ilikuwa mwezi Desemba mwaka 2004. Mara ile Osama alitamka kumuunga mkono aliyemwiita shujaa Abu Musab Zarqawi wa Iraq na kuwahamasisha Wairak kugomea majaribio yenye kupelekea chaguzi za kidemokrasia katika Iraq.

Lakini, mwaka ule wa 2006, Osama Bin Laden alijitokeza na sura nyingine kabisa. Si Osama yule tuliyemzoea na sura yake ya kwanza ya Osama gaidi. Tulimwona Osama bin Laden aliyesikika zaidi kama mwanasiasa, mpatanishi wa amani.

Katika kauli ile ya Osama, kama ilivyotarajiwa alitishia kuishambulia Marekani ndani ya ardhi yake. "Matayarisho yetu yako mbioni, nanyi (Wamarekani) mtashuhudia hayo mara yatakapokamilika" Alisema Osama.

Pamoja na Osama kutoa tishio hilo kwa Marekani, katika hali isiyo ya kawaida kwa kiongozi wa kikundi cha kigaidi, Osama alikaribisha upatanisho kwa maana ya pande mbili kufanya mazungumzo ya kusimamisha mapambano. Katika hili, Osama alitoa masharti ya kufikiwa makubaliano hayo ya kusimamisha mapambano.

"Ondokeni Iraq na Afghanstan, ndipo hapo wapiganaji wetu wa Mungu watapoiacha miji yenu katika amani. Kwa namna hiyo pande zote mbili zitanufaika na hali ya amani na utulivu. Hivyo basi tunaweza kuijenga Iraq na Afghanstan” Alisema Bin Laden.

Bila shaka, Osama Bin Laden kwa kuyasema hayo hakuwa na matarajio kuwa utawala wa Rais George Bush ungeyakubali kirahisi mapendekezo yake, maana, kauli ya Osama ilijaa hila na ghilba.

Vivyo hivyo, kwa nchi za Kimagharibi ambazo mwaka 2004 Osama alipata kuzitupia nyavu zikubaliane na Al Qaida kusitisha mapambano kwa miezi mitatu lakini nchi hizo zilikataa. Na hata mwaka ule wa 2006 , utawala wa Bush ulitoa jibu la haraka juu ya mapendekezo ya Osama Bin Laden. "Hatujadiliani na magaidi". Ilisema Marekani.

Kilichojitokeza ni kwa vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu kuuweka upinzani dhidi ya Marekani katika Iraq katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile "linalokubalika". Ni kundi la upinzani unaondeshwa na jumuiya za kisiasa ikiwemo vyama vu kisiasa. Na kundi la pili ni lile "lisilokubalika". Hili ni kundi la upinzani linaloendesha harakati zake dhidi ya Marekani kijeshi na kwa mbinu za kigaidi.

Chochote kinachonukia Al Qaida kinaingizwa katika kundi la pili. Hali hiyo ilipelekea nyota ya Osama Bin laden kufifia katika ulimwengu wa Waislamu. Na ukawa mwanzo wa anguko la Osama Bin Laden.

Ni nini kitafuatia, na tusubiri tuone.
Maggid,
Iringa
Jumatatu, Mei 2, 2011