Kiongozi wa Libya, Kanali Gaddafi, ametoa wito kwa Nato kwamba kufanywe mazungumzo ili kusimamisha mashambulio ya ndege za umoja huo dhidi ya nchi yake. Katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni, Kanali Gaddafi alisema yeye yuko tayari kusimamisha mapigano ikiwa itakubaliwa na pande zote. Katika hotuba yake Jumamosi asubuhi, kiongozi wa Libya alisema yuko tayari kutoa amri kuwa mapigano yasitishwe na kuanza mazungumzo, endapo NATO itaacha mashambulio ya mabomu. Lakini alikataa lile dai kubwa la wapiganaji na jumuiya ya kimataifa, kwamba yeye aondoke. Alisema hatong'atuka wala kuihama Libya. Wengi serikalini wanaona kuwa wameshakaribisha mazungumzo kwa kukubali mpago wa Umoja wa Afrika wa kurejesha amani; lakini wanahisi upinzani ndio hautaki kumaliza mapigano, kwa sababu unakataa kuzungumza na serikali ya Kanali Gaddafi. Alipokuwa Kanali Gaddafi anazungumza, NATO ilidondosha makombora matatu mjini Tripoli, kwenye yale yaliyoonekana kama majengo ya serikali. Hotuba ya Kanali Gaddafi, ilikuwa mchanganyiko wa kukaza na kulegeza kamba. Alisema kila mwananchi wa Libya sasa anakabili mambo mawili : uhuru ama kifo. Hakuna kusalliam amri, hakuna hofu wala kuondoka. |